Chakula cha Nguruwe: Mwongozo Kamili wa Formula za Kilo 10, 50 na 100
Kutoka kitoto kinachonyonya mpaka nguruwe wa kilo tisini. Bonyeza jina la chakula unalotaka, jedwali lake litafunguka papo hapo.
- Ngazi saba: Creep, Weaner, Grower, Finisher, Mimba, Kunyonyesha, Dume
- Kila ngazi ina toleo la formula kamili na toleo la kijijini
- Mbadala wa kila malighafi unayokosa
- Mabaki ya hotelini: jinsi ya kuyatumia bila kuua nguruwe wako
- Vipimo, bei na hesabu ya faida kwa mwaka
Mwongozo huu umeandikwa kwa mfugaji mwenye nguruwe 2 mpaka 50, asiye na mashine, anayenunua sokoni la kijiji au dukani.
1Anza hapa
Nguruwe ni mfugo wa faida kubwa kuliko wengi. Anazaa vitoto kumi kwa mara moja, mara mbili kwa mwaka, na anafikia kilo tisini ndani ya miezi sita. Lakini chakula huchukua asilimia sabini na tano ya gharama zote. Ukikosea hapa, faida yote inaisha.
Tofauti kubwa kati ya nguruwe na kuku ni hii: nguruwe ana tumbo moja kama binadamu. Hawezi kumeng’enya majani mengi kama ng’ombe. Ukimpa pumba peke yake atakula sana na kubaki mwembamba. Anahitaji protini halisi.
Vitu vitano vya kuvielewa kabla ya kuchanganya
| Kitu | Kinatoka wapi | Kazi yake | Kikikosekana |
|---|---|---|---|
| Nishati | Mahindi, mtama, mihogo, molasi | Huleta unene wa nyama | Nguruwe hula sana bila kukua |
| Protini | Soya, alizeti, dagaa, unga wa samaki, maharage | Hujenga misuli, si mafuta | Ukuaji hudumaa, mifupa hubaki mikubwa kuliko nyama |
| Lysine | Soya, dagaa, unga wa samaki | Amino asidi muhimu kuliko zote kwa nguruwe | Hakui hata ukimpa protini nyingi |
| Kalsiamu na fosforasi | Chokaa, maganda ya mayai, mifupa, DCP | Hujenga mifupa na maziwa ya jike | Nguruwe wa kilo 70 huvunjika mguu |
| Nyuzi | Pumba, majani makavu | Humshibisha jike mwenye mimba bila kumnenepesha | Jike hunenepa na kushindwa kuzaa vizuri |
2Ngazi saba za chakula
| Ngazi | Umri au uzito | Protini | Kiasi kwa siku |
|---|---|---|---|
| A. Creep vitoto vinavyonyonya | Siku 7 hadi kuachishwa. Kilo 1.5 hadi 8. | 20% hadi 22% | Gramu 50 hadi 300 |
| B. Weaner baada ya kuachishwa | Wiki 8 hadi 14. Kilo 8 hadi 20. | 18% hadi 20% | Kilo 0.6 hadi 1.0 |
| C. Grower anayekua | Kilo 20 hadi 50 | 16% hadi 18% | Kilo 1.2 hadi 2.0 |
| D. Finisher kunenepesha | Kilo 50 hadi 90 | 14% hadi 15% | Kilo 2.2 hadi 3.0 |
| E. Mimba jike mwenye mimba | Siku 114 za mimba | 14% | Kilo 2.0 hadi 2.5 |
| F. Kunyonyesha jike anayenyonyesha | Kuzaa hadi kuachisha | 16% hadi 18% | Kilo 4.0 hadi 6.0 |
| G. Dume wa mbegu | Mwaka mzima | 15% | Kilo 2.0 hadi 2.5 |
3Chagua chakula
Bonyeza jina la chakula unalotaka kuchanganya. Kila jedwali linaonyesha kilo 10, kilo 50 na kilo 100, pamoja na safu ya njano ya mbadala wa kila malighafi.
Creep: chakula cha vitoto vinavyonyonya
| Wakati | Siku 7 hadi kuachishwa | Uzito | Kilo 1.5 hadi 8 |
|---|---|---|---|
| Protini | 20% – 22% | Chakula kwa siku | Gramu 50 – 300 |
| Maji kwa siku | Lita 1 | Toleo | Kamili au la kijijini |
Kitoto kinachonyonya hupata maziwa ya kutosha wiki mbili za mwanzo tu. Baada ya hapo maziwa ya mama hayatoshi. Weka chakula hiki kwenye chombo kidogo ndani ya eneo ambalo mama hawezi kufika.
TOLEO LA 1Ina premix ya nguruwe, soya, DCP na lysine
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 5.1 kg | 25.5 kg | 51 kg | Mtama kilo kwa kilo. Mihogo isizidi kilo 8, vitoto hawavumilii. |
| Pumba za ngano au za mahindi | 600 g | 3 kg | 6 kg | Pumba za mpunga zisizidi kilo 4. Ni ngumu kwa tumbo la kitoto. |
| Mashudu ya soya (yaliyochomwa) | 2 kg | 10 kg | 20 kg | Mashudu ya alizeti kilo 26 na punguza mahindi kilo 6. |
| Mashudu ya alizeti | 800 g | 4 kg | 8 kg | Ongeza mashudu ya soya kilo 6 na mahindi kilo 2. |
| Unga wa samaki au dagaa | 800 g | 4 kg | 8 kg | Vichwa vya samaki vilivyochemshwa na kukaushwa. Au maziwa ya unga ya ndama. |
| Molasi (miwa) | 300 g | 1.5 kg | 3 kg | Ongeza mahindi kilo 3. Molasi huvutia kitoto kula mapema. |
| DCP au unga wa mifupa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Unga wa mifupa uliochomwa kilo 1.5 badala ya kilo 1 ya DCP. |
| Chokaa ya kulisha | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Maganda ya mayai yaliyosagwa laini kilo kwa kilo. |
| Chumvi ya mezani | 30 g | 150 g | 300 g | Hakuna mbadala. Usizidishe, nguruwe hufa kwa chumvi nyingi. |
| Premix ya nguruwe | 50 g | 250 g | 500 g | Majani ya mlonge yaliyokaushwa kilo 2, pamoja na vitamini za maji. |
| Lysine | 15 g | 75 g | 150 g | Ongeza mashudu ya soya kilo 1.5 na punguza mahindi kilo 1.5. |
| Methionine | 5 g | 25 g | 50 g | Ongeza unga wa samaki gramu 500. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 20.8%
TOLEO LA 2Bila premix, bila DCP, bila soya
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 4.7 kg | 23.5 kg | 47 kg | Mtama au uwele kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 800 g | 4 kg | 8 kg | Pumba za mpunga zisizidi kilo 4. |
| Mashudu ya alizeti | 2.2 kg | 11 kg | 22 kg | Mashudu ya ufuta kilo kwa kilo. |
| Dagaa waliosagwa | 1.3 kg | 6.5 kg | 13 kg | Vichwa na matumbo ya samaki vilivyochemshwa na kukaushwa. |
| Maharage au kunde zilizochemshwa | 400 g | 2 kg | 4 kg | Mbaazi zilizochemshwa. Mbichi ni sumu. |
| Unga wa mifupa uliochomwa | 200 g | 1 kg | 2 kg | Mifupa ya mnadani, chomwa hadi myeupe kisha saga. |
| Maganda ya mayai yaliyosagwa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Chokaa ya jiwe iliyosagwa laini. |
| Majani makavu ya mlonge au matembele | 200 g | 1 kg | 2 kg | Majani ya mihogo yaliyokaushwa kivulini. |
| Chumvi ya mezani | 50 g | 250 g | 500 g | Hakuna mbadala. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 20%
Weaner: baada ya kuachishwa
| Wakati | Wiki 8 hadi 14 | Uzito | Kilo 8 hadi 20 |
|---|---|---|---|
| Protini | 18% – 20% | Chakula kwa siku | Kilo 0.6 – 1.0 |
| Maji kwa siku | Lita 2 – 4 | Toleo | Kamili au la kijijini |
Wiki mbili za mwanzo baada ya kuachishwa ndizo hatari zaidi maishani mwa nguruwe. Kitoto kinaacha maziwa ghafla, kinatengwa na mama, na kinaingia kwenye banda jipya.
TOLEO LA 1Ina premix ya nguruwe, soya, DCP na lysine
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 5.6 kg | 28 kg | 56 kg | Mtama kilo kwa kilo. Mihogo isizidi kilo 12. |
| Pumba za mahindi | 1 kg | 5 kg | 10 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya soya | 1.7 kg | 8.5 kg | 17 kg | Mashudu ya alizeti kilo 22 na punguza mahindi kilo 5. |
| Mashudu ya alizeti | 800 g | 4 kg | 8 kg | Ongeza soya kilo 6 na mahindi kilo 2. |
| Unga wa samaki au dagaa | 500 g | 2.5 kg | 5 kg | Funza wa nzi mweusi au vichwa vya samaki. |
| DCP au unga wa mifupa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Unga wa mifupa uliochomwa. |
| Chokaa ya kulisha | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Maganda ya mayai yaliyosagwa. |
| Chumvi ya mezani | 30 g | 150 g | 300 g | Hakuna mbadala. |
| Premix ya nguruwe | 50 g | 250 g | 500 g | Majani makavu ya mlonge kilo 2. |
| Lysine | 20 g | 100 g | 200 g | Ongeza mashudu ya soya kilo 1.5. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 18.6%
TOLEO LA 2Bila premix, bila DCP, bila soya
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 5.1 kg | 25.5 kg | 51 kg | Mtama, uwele au mihogo isizidi kilo 12. |
| Pumba za mahindi | 1.2 kg | 6 kg | 12 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya alizeti | 2 kg | 10 kg | 20 kg | Mashudu ya ufuta kilo kwa kilo. |
| Dagaa waliosagwa | 1 kg | 5 kg | 10 kg | Vichwa vya samaki, funza wa nzi mweusi, au mchwa. |
| Maharage au kunde zilizochemshwa | 200 g | 1 kg | 2 kg | Mbaazi zilizochemshwa na kusagwa. |
| Unga wa mifupa uliochomwa | 200 g | 1 kg | 2 kg | Mifupa ya mnadani iliyochomwa. |
| Maganda ya mayai yaliyosagwa | 100 g | 500 g | 1 kg | Chokaa ya jiwe laini. |
| Majani makavu ya matembele | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Majani ya mihogo au mlonge yaliyokaushwa kivulini. |
| Chumvi ya mezani | 50 g | 250 g | 500 g | Hakuna mbadala. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 18.1%
Grower: nguruwe anayekua
| Wakati | Miezi 3 hadi 4 | Uzito | Kilo 20 hadi 50 |
|---|---|---|---|
| Protini | 16% – 18% | Chakula kwa siku | Kilo 1.2 – 2.0 |
| Maji kwa siku | Lita 5 – 8 | Toleo | Kamili au la kijijini |
Hapa ndipo nguruwe anakua haraka kuliko wakati wowote. Anaongeza gramu mia sita hadi mia saba kwa siku akipata chakula sahihi. Usipunguze protini hapa kwa kutaka kuokoa pesa.
TOLEO LA 1Ina premix ya nguruwe, soya, DCP na lysine
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 5.7 kg | 28.5 kg | 57 kg | Mtama kilo kwa kilo. Mihogo mikavu isizidi kilo 20. |
| Pumba za mahindi | 1.4 kg | 7 kg | 14 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya soya | 1.3 kg | 6.5 kg | 13 kg | Mashudu ya alizeti kilo 17 na punguza mahindi kilo 4. |
| Mashudu ya alizeti | 1 kg | 5 kg | 10 kg | Mashudu ya pamba kilo 5 tu, si zaidi. |
| Unga wa samaki au dagaa | 200 g | 1 kg | 2 kg | Funza wa nzi mweusi au machicha ya pombe yaliyokaushwa kilo 4. |
| DCP au unga wa mifupa | 140 g | 700 g | 1.4 kg | Unga wa mifupa uliochomwa. |
| Chokaa ya kulisha | 180 g | 900 g | 1.8 kg | Maganda ya mayai yaliyosagwa. |
| Chumvi ya mezani | 30 g | 150 g | 300 g | Hakuna mbadala. |
| Premix ya nguruwe | 40 g | 200 g | 400 g | Majani makavu ya mlonge kilo 2. |
| Lysine | 10 g | 50 g | 100 g | Ongeza mashudu ya soya kilo 0.8. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 16.4%
TOLEO LA 2Bila premix, bila DCP, bila soya
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 4.6 kg | 23 kg | 46 kg | Mtama au uwele kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 1.8 kg | 9 kg | 18 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mihogo mikavu iliyosagwa | 600 g | 3 kg | 6 kg | Ongeza mahindi kilo 6. Mihogo lazima ilowekwe na kuanikwa. |
| Mashudu ya alizeti | 1.8 kg | 9 kg | 18 kg | Mashudu ya ufuta. Au mashudu ya pamba kilo 5 na alizeti kilo 13. |
| Dagaa waliosagwa | 700 g | 3.5 kg | 7 kg | Machicha ya pombe yaliyokaushwa kilo 12, punguza pumba kilo 5. |
| Unga wa mifupa uliochomwa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Mifupa ya mnadani iliyochomwa. |
| Maganda ya mayai yaliyosagwa | 100 g | 500 g | 1 kg | Chokaa ya jiwe iliyosagwa laini. |
| Majani makavu ya matembele | 200 g | 1 kg | 2 kg | Majani ya mihogo au mlonge yaliyokaushwa kivulini. |
| Chumvi ya mezani | 50 g | 250 g | 500 g | Hakuna mbadala. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 16%
Finisher: kunenepesha kabla ya kuuza
| Wakati | Miezi 4 hadi 6 | Uzito | Kilo 50 hadi 90 |
|---|---|---|---|
| Protini | 14% – 15% | Chakula kwa siku | Kilo 2.2 – 3.0 |
| Maji kwa siku | Lita 8 – 12 | Toleo | Kamili au la kijijini |
Lengo hapa ni unene wa nyama, si mifupa. Protini inashuka, nishati inapanda. Usimpe unga wa samaki mwingi hapa, nyama itanuka samaki na mnunuzi atakukataa.
TOLEO LA 1Ina premix ya nguruwe, soya, DCP na lysine
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 6.1 kg | 30.5 kg | 61 kg | Mtama kilo kwa kilo. Mihogo mikavu isizidi kilo 25. |
| Pumba za mahindi | 1.6 kg | 8 kg | 16 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya soya | 1 kg | 5 kg | 10 kg | Mashudu ya alizeti kilo 13 na punguza mahindi kilo 3. |
| Mashudu ya alizeti | 900 g | 4.5 kg | 9 kg | Mashudu ya pamba kilo 5 tu. |
| DCP au unga wa mifupa | 140 g | 700 g | 1.4 kg | Unga wa mifupa uliochomwa. |
| Chokaa ya kulisha | 180 g | 900 g | 1.8 kg | Maganda ya mayai yaliyosagwa. |
| Chumvi ya mezani | 30 g | 150 g | 300 g | Hakuna mbadala. |
| Premix ya nguruwe | 40 g | 200 g | 400 g | Majani makavu ya mlonge kilo 2. |
| Lysine | 10 g | 50 g | 100 g | Ongeza mashudu ya soya kilo 0.8. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 14.2%
TOLEO LA 2Bila premix, bila DCP, bila soya
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 4.8 kg | 24 kg | 48 kg | Mtama au uwele kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 2 kg | 10 kg | 20 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mihogo mikavu iliyosagwa | 800 g | 4 kg | 8 kg | Ongeza mahindi kilo 8. |
| Mashudu ya alizeti | 1.4 kg | 7 kg | 14 kg | Mashudu ya ufuta kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya pamba | 300 g | 1.5 kg | 3 kg | Ongeza mashudu ya alizeti kilo 3 badala yake. |
| Dagaa waliosagwa | 400 g | 2 kg | 4 kg | Machicha ya pombe yaliyokaushwa kilo 7, punguza pumba kilo 3. |
| Unga wa mifupa uliochomwa | 120 g | 600 g | 1.2 kg | Mifupa ya mnadani iliyochomwa. |
| Maganda ya mayai yaliyosagwa | 100 g | 500 g | 1 kg | Chokaa ya jiwe laini. |
| Majani makavu ya matembele | 30 g | 150 g | 300 g | Majani ya mihogo yaliyokaushwa. |
| Chumvi ya mezani | 50 g | 250 g | 500 g | Hakuna mbadala. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 14.2%
Nguruwe jike mwenye mimba
| Wakati | Siku 114 za mimba | Uzito | Kilo 120 hadi 180 |
|---|---|---|---|
| Protini | 14% | Chakula kwa siku | Kilo 2.0 – 2.5 |
| Maji kwa siku | Lita 12 – 15 | Toleo | Kamili au la kijijini |
Nguruwe jike mwenye mimba akinenepa atapata shida ya kuzaa na atazaa vitoto vichache. Chakula hiki kina pumba nyingi ili ashibe bila kunenepa. Mpe kilo mbili tu kwa siku, hata akilia.
TOLEO LA 1Ina premix ya nguruwe, soya, DCP na lysine
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 4.8 kg | 24 kg | 48 kg | Mtama kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 2.8 kg | 14 kg | 28 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. Hapa pumba nyingi ni nzuri, humzuia kunenepa. |
| Mashudu ya alizeti | 1.3 kg | 6.5 kg | 13 kg | Mashudu ya ufuta kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya soya | 600 g | 3 kg | 6 kg | Mashudu ya alizeti kilo 8 na punguza mahindi kilo 2. |
| DCP au unga wa mifupa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Unga wa mifupa uliochomwa. |
| Chokaa ya kulisha | 250 g | 1.25 kg | 2.5 kg | Maganda ya mayai yaliyosagwa. |
| Chumvi ya mezani | 35 g | 175 g | 350 g | Hakuna mbadala. |
| Premix ya nguruwe | 50 g | 250 g | 500 g | Majani makavu ya mlonge kilo 2. |
| Lysine | 15 g | 75 g | 150 g | Ongeza mashudu ya soya kilo 1. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 14%
TOLEO LA 2Bila premix, bila DCP, bila soya
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 4.1 kg | 20.5 kg | 41 kg | Mtama au uwele kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 3 kg | 15 kg | 30 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mihogo mikavu iliyosagwa | 600 g | 3 kg | 6 kg | Ongeza mahindi kilo 6. |
| Mashudu ya alizeti | 1.2 kg | 6 kg | 12 kg | Mashudu ya ufuta kilo kwa kilo. |
| Dagaa waliosagwa | 400 g | 2 kg | 4 kg | Machicha ya pombe yaliyokaushwa kilo 7. |
| Majani makavu ya matembele au mihogo | 350 g | 1.75 kg | 3.5 kg | Majani ya mlonge au lusina yaliyokaushwa kivulini. |
| Unga wa mifupa uliochomwa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Mifupa ya mnadani iliyochomwa. |
| Maganda ya mayai yaliyosagwa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Chokaa ya jiwe laini. |
| Chumvi ya mezani | 50 g | 250 g | 500 g | Hakuna mbadala. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 13.9%
Nguruwe anayenyonyesha
| Wakati | Kuzaa hadi kuachisha | Uzito | Kilo 130 hadi 200 |
|---|---|---|---|
| Protini | 16% – 18% | Chakula kwa siku | Kilo 4.0 – 6.0 |
| Maji kwa siku | Lita 25 – 35 | Toleo | Kamili au la kijijini |
Nguruwe anayenyonyesha vitoto kumi hutoa lita nane za maziwa kwa siku. Hii ni kazi kubwa kuliko yoyote mwilini. Mpe chakula kingi kadri anavyoweza kula, hakuna kikomo hapa.
TOLEO LA 1Ina premix ya nguruwe, soya, DCP na lysine
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 5.7 kg | 28.5 kg | 57 kg | Mtama kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 1.2 kg | 6 kg | 12 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya soya | 1.4 kg | 7 kg | 14 kg | Mashudu ya alizeti kilo 18 na punguza mahindi kilo 4. |
| Mashudu ya alizeti | 800 g | 4 kg | 8 kg | Ongeza soya kilo 6 na mahindi kilo 2. |
| Unga wa samaki au dagaa | 300 g | 1.5 kg | 3 kg | Funza wa nzi mweusi au vichwa vya samaki. |
| Molasi (miwa) | 200 g | 1 kg | 2 kg | Ongeza mahindi kilo 2. Molasi humpa nguvu ya kutoa maziwa. |
| DCP au unga wa mifupa | 140 g | 700 g | 1.4 kg | Unga wa mifupa uliochomwa. |
| Chokaa ya kulisha | 180 g | 900 g | 1.8 kg | Maganda ya mayai yaliyosagwa. |
| Chumvi ya mezani | 30 g | 150 g | 300 g | Hakuna mbadala. |
| Premix ya nguruwe | 40 g | 200 g | 400 g | Majani makavu ya mlonge kilo 2. |
| Lysine | 10 g | 50 g | 100 g | Ongeza mashudu ya soya kilo 0.8. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 16.6%
TOLEO LA 2Bila premix, bila DCP, bila soya
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 5.1 kg | 25.5 kg | 51 kg | Mtama au uwele kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 1.4 kg | 7 kg | 14 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya alizeti | 1.8 kg | 9 kg | 18 kg | Mashudu ya ufuta kilo kwa kilo. |
| Dagaa waliosagwa | 900 g | 4.5 kg | 9 kg | Vichwa vya samaki vilivyochemshwa na kukaushwa. |
| Maharage au kunde zilizochemshwa | 200 g | 1 kg | 2 kg | Mbaazi zilizochemshwa na kusagwa. |
| Unga wa mifupa uliochomwa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Mifupa ya mnadani iliyochomwa. |
| Maganda ya mayai yaliyosagwa | 200 g | 1 kg | 2 kg | Chokaa ya jiwe laini. |
| Majani makavu ya matembele | 200 g | 1 kg | 2 kg | Majani ya mlonge au mihogo yaliyokaushwa kivulini. |
| Chumvi ya mezani | 50 g | 250 g | 500 g | Hakuna mbadala. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 17.3%
Hesabu ya chakula cha anayenyonyesha
Anza na kilo mbili siku ya kuzaa. Ongeza nusu kilo kila siku mpaka siku ya saba. Kuanzia hapo, mpe kilo mbili pamoja na gramu mia nne kwa kila kitoto anachonyonyesha.
Mfano: nguruwe mwenye vitoto kumi anahitaji kilo mbili pamoja na kilo nne, jumla kilo sita kwa siku. Agawanye mara tatu: asubuhi, mchana na jioni.
Siku tatu kabla ya kuachisha, punguza chakula kwa nusu. Hii husaidia maziwa kukauka bila maumivu ya matiti.
Nguruwe dume wa mbegu
| Wakati | Mwaka mzima | Uzito | Kilo 150 hadi 250 |
|---|---|---|---|
| Protini | 15% | Chakula kwa siku | Kilo 2.0 – 2.5 |
| Maji kwa siku | Lita 10 – 12 | Toleo | Kamili au la kijijini |
Nguruwe dume mnene hushindwa kupanda na hupunguza mbegu. Mpe kilo mbili tu kwa siku, ongeza nusu kilo msimu wa kupanda.
TOLEO LA 1Ina premix ya nguruwe, soya, DCP na lysine
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 5.3 kg | 26.5 kg | 53 kg | Mtama kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 2.2 kg | 11 kg | 22 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mashudu ya soya | 1.1 kg | 5.5 kg | 11 kg | Mashudu ya alizeti kilo 14 na punguza mahindi kilo 3. |
| Mashudu ya alizeti | 1 kg | 5 kg | 10 kg | Mashudu ya ufuta kilo kwa kilo. |
| DCP au unga wa mifupa | 140 g | 700 g | 1.4 kg | Unga wa mifupa uliochomwa. |
| Chokaa ya kulisha | 180 g | 900 g | 1.8 kg | Maganda ya mayai yaliyosagwa. |
| Chumvi ya mezani | 30 g | 150 g | 300 g | Hakuna mbadala. |
| Premix ya nguruwe | 40 g | 200 g | 400 g | Majani makavu ya mlonge kilo 2. |
| Lysine | 10 g | 50 g | 100 g | Ongeza mashudu ya soya kilo 0.8. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 15%
TOLEO LA 2Bila premix, bila DCP, bila soya
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 4.5 kg | 22.5 kg | 45 kg | Mtama au uwele kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 2.4 kg | 12 kg | 24 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Mihogo mikavu iliyosagwa | 500 g | 2.5 kg | 5 kg | Ongeza mahindi kilo 5. |
| Mashudu ya alizeti | 1.7 kg | 8.5 kg | 17 kg | Mashudu ya ufuta kilo kwa kilo. |
| Dagaa waliosagwa | 500 g | 2.5 kg | 5 kg | Machicha ya pombe yaliyokaushwa kilo 9. |
| Unga wa mifupa uliochomwa | 150 g | 750 g | 1.5 kg | Mifupa ya mnadani iliyochomwa. |
| Maganda ya mayai yaliyosagwa | 100 g | 500 g | 1 kg | Chokaa ya jiwe laini. |
| Majani makavu ya matembele | 100 g | 500 g | 1 kg | Majani ya mlonge yaliyokaushwa kivulini. |
| Chumvi ya mezani | 50 g | 250 g | 500 g | Hakuna mbadala. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 15%
4Jedwali kubwa la mbadala
Tafuta kile unachokosa kwenye safu ya kwanza, kisha soma kulia.
| Unachokosa | Kwa nini kinahitajika | Mbadala wa kwanza | Mbadala wa pili | Marekebisho ya kiasi |
|---|---|---|---|---|
| Mashudu ya soya | Protini na lysine. Ndiyo malighafi bora kuliko zote kwa nguruwe. | Mashudu ya alizeti | Maharage, kunde au mbaazi zilizochemshwa dakika 30, kukaushwa na kusagwa | Kilo 3 za alizeti badala ya kilo 2 za soya, punguza mahindi kilo 1. |
| Premix ya nguruwe | Vitamini A, D, E, B12, shaba na zinki | Majani ya mlonge, matembele au mihogo yaliyokaushwa kivulini na kusagwa, kilo 2 | Vitamini za maji za mifugo, mara mbili kwa wiki, pamoja na kuwaachia nje kwenye jua | Gramu 400 hadi 500 za premix zinabadilishwa na kilo 2 za majani makavu. |
| Lysine | Amino asidi muhimu kuliko zote kwa nguruwe. Bila yo hakui. | Ongeza mashudu ya soya | Ongeza dagaa au unga wa samaki | Gramu 100 za lysine zinabadilishwa na kilo 0.8 za soya, au kilo 1 ya dagaa. |
| DCP | Fosforasi ya mifupa. Nguruwe mzito mwenye mifupa dhaifu huvunjika miguu. | Unga wa mifupa uliochomwa hadi myeupe kisha kusagwa | Ongeza dagaa au vichwa vya samaki vilivyosagwa | Unga wa mifupa kilo 1.5 badala ya kilo 1 ya DCP. |
| Chokaa ya kulisha | Kalsiamu ya mifupa na maziwa ya nguruwe jike | Maganda ya mayai yaliyooshwa, kuchemshwa, kukaushwa na kusagwa laini | Chokaa ya jiwe ya maduka ya ujenzi, iliyosagwa laini kama unga | Kilo 1 badala ya kilo 1. |
| Unga wa samaki | Protini ya wanyama na lysine | Dagaa wa ziwani waliosagwa | Vichwa na matumbo ya samaki vilivyochemshwa, kukaushwa juani na kusagwa. Au funza wa nzi mweusi. | Kilo 1 badala ya kilo 1. Kwa Finisher usizidi kilo 3, nyama itanuka. |
| Mahindi | Nishati, msingi wa chakula | Mtama au uwele, kilo kwa kilo | Mihogo mikavu iliyolowekwa siku tatu na kuanikwa juani. Au viazi vitamu vilivyokaushwa. | Mihogo isizidi robo ya mchanganyiko kwa nguruwe wakubwa, kilo 8 tu kwa vitoto. Ongeza dagaa kilo 2. |
| Pumba za mahindi | Nyuzi na nishati ya bei nafuu | Pumba za mpunga | Machicha ya pombe yaliyokaushwa juani. Au maganda ya alizeti yaliyosagwa. | Machicha makavu kilo 1 badala ya pumba kilo 1. Machicha mabichi kilo 3 badala ya kilo 1. |
| Chanzo cha protini chochote | Kujenga misuli | Machicha ya pombe ya mtama au mahindi, yaliyokaushwa | Funza wa nzi mweusi, minyoo ya kufuga, au mchwa waliokaushwa | Machicha makavu kilo 12 badala ya dagaa kilo 7, punguza pumba kilo 5. |
| Molasi | Nishati ya haraka na ladha nzuri | Ongeza mahindi kiasi kile kile | Maji ya sukari ya miwa yaliyochemshwa, au viazi vitamu vilivyochemshwa | Molasi isizidi kilo 5 kwa kila kilo 100, huleta kuharisha. |
| Majani ya kijani | Vitamini na nyuzi, hupunguza gharama | Matembele, majani ya mihogo, mlonge au lusina | Majani ya maboga, mabaki ya mboga za sokoni | Mabichi kilo 3 hadi 5 kwa siku kwa nguruwe mkubwa, wape kando si kwenye mchanganyiko. |
| Chumvi | Hamu ya kula na uwiano wa maji mwilini | Hakuna mbadala. Ipo kila duka. | Usitumie chumvichumvi ya samaki wala chumvi ya mifugo yenye madini mengine. | Gramu 300 hadi 500 kwa kilo 100. Kuzidisha huua nguruwe hasa akikosa maji. |
5Mabaki ya jikoni na hotelini
Mabaki ya chakula ni nafuu na yanapatikana kila mji. Yanaweza kupunguza gharama yako kwa nusu. Lakini ndiyo njia kuu ya kusambaza homa ya nguruwe ya Afrika, ugonjwa unaoua kundi lote ndani ya wiki moja na hauna dawa wala chanjo.
Kanuni saba za mabaki
| Kanuni | Kwa nini |
|---|---|
| Chemsha dakika 30, kisha acha yapoe | Huua virusi vya homa ya nguruwe ya Afrika na bakteria wengine |
| Kamwe usiwape mabaki yenye nyama ya nguruwe, soseji au bacon | Ndiyo chanzo hatari kuliko chote, hata yakichemshwa |
| Ondoa mifupa mikali, chuma, plastiki na karatasi za kufungia | Huchana utumbo na huua ndani ya siku mbili |
| Usiwape mabaki yaliyooza au yenye ukungu | Nguruwe ni nyeti kwa aflatoksini kuliko kuku |
| Changanya na pumba na dagaa, si mabaki peke yake | Mabaki yana maji mengi na protini kidogo |
| Kwa kila debe la mabaki, ongeza kilo 2 za mchanganyiko kavu wa Grower | Kurudisha uwiano wa protini na nishati |
| Usiwape majike wenye mimba wiki mbili za mwisho, wala vitoto chini ya kilo 20 | Tumbo lao haliwezi kuhimili mabadiliko ya ghafla |
6Nina vitu vitatu tu, nifanyeje
Unayo mahindi, pumba na dagaa peke yake. Hakuna alizeti sokoni, hakuna pesa ya premix. Usisimamishe kulisha. Tumia mchanganyiko huu kwa nguruwe wa kilo ishirini na kuendelea.
| Malighafi | Kilo 10 | Kilo 50 | Kilo 100 | Kama huna, tumia |
|---|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 5.5 kg | 27.5 kg | 55 kg | Mtama au uwele kilo kwa kilo. |
| Pumba za mahindi | 3 kg | 15 kg | 30 kg | Pumba za mpunga kilo kwa kilo. |
| Dagaa waliosagwa | 1.5 kg | 7.5 kg | 15 kg | Vichwa vya samaki, machicha ya pombe yaliyokaushwa kilo 25 na punguza pumba kilo 10. |
| JUMLA | 10.00 kg | 50.00 kg | 100.00 kg |
Protini iliyopatikana: takribani 16.5%
Mapungufu ya mchanganyiko huu
| Pungufu | Kitakachotokea | Muda |
|---|---|---|
| Kalsiamu haitoshi | Nguruwe wa kilo 70 anaweza kuvunjika mguu | Baada ya miezi 3 |
| Hakuna vitamini | Manyoya magumu, ngozi kavu, ukuaji wa polepole | Baada ya mwezi 1 |
| Dagaa ni ghali | Kilo 100 itakugharimu zaidi ya formula ya kijijini yenye alizeti | Mara moja |
Nini uongeze mara tu unapopata
| Hatua | Ongeza | Punguza | Gharama |
|---|---|---|---|
| 1 | Maganda ya mayai kilo 2 na unga wa mifupa kilo 1.5 | Pumba kilo 3.5 | Karibu bure |
| 2 | Majani makavu ya matembele au mlonge kilo 2 | Mahindi kilo 2 | Bure |
| 3 | Chumvi gramu 500 | Hakuna | TSh 500 |
| 4 | Mashudu ya alizeti kilo 18 | Dagaa kilo 8 na mahindi kilo 10 | Hupunguza gharama |
Ukifanya hatua zote nne, umefika kwenye formula ya kijijini ya Grower.
7Bajeti yako ikoje
| Bajeti ndogo | Bajeti ya kati | Bajeti kamili | |
|---|---|---|---|
| Unachonunua | Mahindi, pumba, dagaa. Mabaki ya hotelini yaliyochemshwa. Vingine unavikusanya. | Mahindi, pumba, alizeti, dagaa, mihogo, unga wa mifupa, chumvi. | Kila kitu pamoja na soya, premix ya nguruwe, lysine na DCP. |
| Formula ya kutumia | Mchanganyiko wa dharura pamoja na mabaki yaliyochemshwa. | Toleo la 2 la kijijini kwa ngazi zote. | Toleo la 1 kamili kwa ngazi zote. |
| Gharama kwa kilo | TSh 900 hadi 1,100 | TSh 950 hadi 1,050 | TSh 1,100 hadi 1,200 |
| Kufikia kilo 90 | Miezi 9 au zaidi | Miezi 7 | Miezi 5.5 hadi 6 |
| Chakula kwa kila kilo ya nyama | Kilo 4.5 au zaidi | Kilo 3.5 | Kilo 3.0 |
| Chakula chote mpaka kuuza | Kilo 400 au zaidi | Kilo 315 | Kilo 270 |
| Vitoto hai kwa mzao | 7 hadi 8 | 9 hadi 10 | 10 hadi 12 |
| Vifo hadi kuachishwa | Asilimia 20 hadi 30 | Asilimia 12 hadi 18 | Chini ya asilimia 10 |
Angalia safu ya chakula chote mpaka kuuza. Bajeti ndogo inaonekana nafuu kwa kilo, lakini inatumia kilo mia moja na thelathini za ziada kwa kila nguruwe. Ukizidisha kwa nguruwe kumi, ni magunia ishirini na sita ya ziada kwa mzunguko mmoja. Hapo ndipo faida inapopotea.
8Kupima bila mizani
Mizani ni bora. Lakini kama huna, vipimo hivi vitakusaidia. Ni kwa malighafi kavu ya kawaida.
| Malighafi | Debe la lita 20 | Ndoo ya lita 10 | Kopo la lita 1 |
|---|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | kilo 12 | kilo 6 | gramu 600 |
| Pumba za mahindi | kilo 7 | kilo 3.5 | gramu 350 |
| Pumba za mpunga | kilo 6 | kilo 3 | gramu 300 |
| Mashudu ya alizeti | kilo 10 | kilo 5 | gramu 500 |
| Mashudu ya soya | kilo 13 | kilo 6.5 | gramu 650 |
| Dagaa waliosagwa | kilo 9 | kilo 4.5 | gramu 450 |
| Mihogo mikavu iliyosagwa | kilo 11 | kilo 5.5 | gramu 550 |
| Machicha ya pombe makavu | kilo 5 | kilo 2.5 | gramu 250 |
| Machicha ya pombe mabichi | kilo 16 | kilo 8 | gramu 800 |
| Unga wa mifupa au chokaa | kilo 18 | kilo 9 | gramu 900 |
| Molasi | kilo 28 | kilo 14 | kilo 1.4 |
| Mabaki ya hotelini yaliyochemshwa | kilo 17 | kilo 8.5 | gramu 850 |
Vitu vidogo: premix, chumvi, lysine
| Kipimo | Premix | Chumvi | Lysine au Methionine |
|---|---|---|---|
| Kijiko cha chakula, kilichojaa | gramu 12 | gramu 18 | gramu 10 |
| Kijiko cha chai, kilichojaa | gramu 4 | gramu 6 | gramu 3.5 |
| Kifuniko cha chupa ya soda | gramu 4 | gramu 5 | gramu 3.5 |
Mfano: kwa kilo 50 za Grower unahitaji gramu 200 za premix. Hivyo ni vijiko vya chakula kumi na saba vilivyojaa.
9Hatua za kuchanganya
| Hatua | Unachofanya | Kwa nini |
|---|---|---|
| 1. Andaa sakafu | Sementi iliyofagiliwa au turubai kubwa iliyotandazwa | Udongo huingiza uchafu, upepo hupeperusha premix |
| 2. Pima kila kitu peke yake | Kila malighafi kwenye rundo lake au ndoo yake kabla ya kumwaga | Hukuzuia kusahau au kurudia malighafi |
| 3. Mwaga vikubwa chini | Mahindi kwanza, kisha pumba, kisha mashudu, kama safu za keki | Rundo bapa huchanganyika kuliko rundo refu |
| 4. Changanya vidogo kwenye ndoo | Pumba kilo 2 pamoja na premix, chumvi na lysine, dakika tatu | Premix ni gramu 400 tu, haiwezi kusambaa yenyewe |
| 5. Mwaga ndoo juu ya rundo | Sambaza juu ya eneo lote, si mahali pamoja | Kuepuka nguruwe mmoja kula premix yote |
| 6. Geuza rundo mara tatu | Kwa koleo, kutoka pembeni peleka katikati, zunguka rundo lote | Mara tatu zinatosha, nyingi zaidi hutenganisha vizito na vyepesi |
| 7. Molasi mwisho kabisa | Ipashe moto iwe nyepesi, inyunyize kwa kopo lenye matundu ukigeuza | Molasi baridi hushikamana na kutengeneza mabonge |
| 8. Fungasha | Mfuko wa plastiki ndani ya gunia, andika tarehe na aina ya chakula | Unyevu huleta ukungu ndani ya siku tano |
10Kiasi cha chakula kwa siku
| Uzito au hali | Chakula kwa siku | Mara ngapi kwa siku | Maji kwa siku |
|---|---|---|---|
| Kitoto kinachonyonya, kilo 1.5 hadi 8 | gramu 50 hadi 300 | Kiwe kipo wakati wote | lita 1 |
| Weaner, kilo 8 hadi 20 | kilo 0.6 hadi 1.0 | Mara 3 | lita 2 hadi 4 |
| Grower, kilo 20 hadi 35 | kilo 1.2 hadi 1.6 | Mara 2 | lita 5 hadi 6 |
| Grower, kilo 35 hadi 50 | kilo 1.6 hadi 2.0 | Mara 2 | lita 6 hadi 8 |
| Finisher, kilo 50 hadi 70 | kilo 2.2 hadi 2.6 | Mara 2 | lita 8 hadi 10 |
| Finisher, kilo 70 hadi 90 | kilo 2.6 hadi 3.0 | Mara 2 | lita 10 hadi 12 |
| Jike mwenye mimba | kilo 2.0 hadi 2.5 | Mara 2 | lita 12 hadi 15 |
| Jike anayenyonyesha | kilo 4.0 hadi 6.0 | Mara 3 | lita 25 hadi 35 |
| Dume wa mbegu | kilo 2.0 hadi 2.5 | Mara 2 | lita 10 hadi 12 |
Hesabu ya nguruwe mmoja mpaka kuuza
Kutoka kuachishwa akiwa kilo nane mpaka kufikia kilo tisini, nguruwe mmoja hula takribani kilo mia mbili sabini za chakula, sawa na magunia matano na nusu ya kilo hamsini.
Kwa gharama ya kutengeneza mwenyewe ya shilingi elfu moja na mia moja kwa kilo, chakula chote ni shilingi laki mbili na tisini na saba elfu. Nguruwe wa kilo tisini anayeuzwa shilingi elfu mia nne na hamsini anakupa faida ya zaidi ya shilingi laki moja baada ya kuondoa gharama ya kitoto na dawa.
Nguruwe kumi kwa mzunguko, mizunguko miwili kwa mwaka, ni magunia mia moja na kumi ya chakula kwa mwaka. Ndiyo maana kuchanganya mwenyewe kunabadilisha kila kitu.
Maji
Nguruwe hunywa lita mbili hadi tatu za maji kwa kila kilo moja ya chakula anachokula. Maji yakikatika, nguruwe huacha kula mara moja na anaweza kupata sumu ya chumvi.
Nguruwe jike anayenyonyesha ndiye anayehitaji maji kuliko wote, lita ishirini na tano hadi thelathini na tano kwa siku. Akikosa maji, maziwa hukauka ndani ya siku moja na vitoto hulia usiku kucha. Weka nipple drinker au ndoo kubwa isiyoweza kupinduliwa.
Osha vyombo vya maji kila siku. Nguruwe hukojoa na kunyea ndani ya maji akiwa na joto, hivyo weka chombo mahali penye kivuli na kiinuliwe kidogo.
11Makosa kumi yanayoua faida
| Kosa | Kinachotokea | Kinga |
|---|---|---|
| 1. Mabaki yasiyochemshwa | Homa ya nguruwe ya Afrika. Kundi lote hufa ndani ya wiki. Hakuna dawa wala chanjo. | Chemsha dakika 30 kila mara, bila kukosa |
| 2. Pumba peke yake | Nguruwe hula sana na kubaki mwembamba miezi kumi | Ongeza mashudu ya alizeti au dagaa |
| 3. Mahindi yenye ukungu | Aflatoksini. Jike hutoa mimba, ini huharibika. | Ukiona doa la kijani au bluu, usinunue hata kwa bei ya bure |
| 4. Chumvi nyingi bila maji | Sumu ya chumvi. Nguruwe huzunguka kama mlevi kisha hufa. | Gramu 5 kwa kilo 1 ya chakula ni kikomo. Maji saa 24. |
| 5. Kunenepesha jike mwenye mimba | Hushindwa kuzaa, huzaa vitoto vichache, hukanyaga vitoto | Kilo 2.5 kwa siku ni kikomo, hata akilia |
| 6. Kubadilisha chakula ghafla | Kuharisha kunakoua, hasa kwa vitoto vilivyoachishwa | Chukua siku tano: robo tatu, nusu, robo, kisha kipya |
| 7. Premix ya kuku kwa nguruwe | Kalsiamu nyingi na dawa za coccidiosis zisizofaa | Tumia premix ya nguruwe, au majani makavu kabisa |
| 8. Soya au maharage mbichi | Kizuizi cha kumeng’enya protini | Choma au chemsha dakika 30 kabla ya kusaga |
| 9. Kusaga laini kupita kiasi | Vidonda vya tumbo | Saga kama mchanga mnene, si kama unga |
| 10. Kuhifadhi zaidi ya mwezi | Vitamini hufa, mafuta ya pumba huwa na uchachu | Changanya kiasi cha wiki nne tu |
12Uhifadhi
| Jambo | Ufanye nini | Kwa nini |
|---|---|---|
| Muda | Changanya kiasi kisichozidi cha wiki nne | Vitamini hufa na mafuta huharibika baada ya hapo |
| Sakafu | Weka magunia juu ya mbao au matofali, nchi nne kutoka chini | Sakafu hupitisha unyevu hata ikiwa kavu kwa juu |
| Ukuta | Acha nafasi ya nchi sita kati ya gunia na ukuta | Hewa ipite, unyevu usikae |
| Chumba | Kiwe na hewa inayopita lakini kisipigwe na mvua | Chumba kilichozibwa hushika joto na unyevu |
| Panya | Weka mtego, si sumu. Kagua magunia kila wiki. | Sumu ikiingia kwenye chakula itaua nguruwe wote |
| Machicha ya pombe | Yatumie siku hiyo hiyo, au anika juani mpaka yakauke kabisa | Mabichi huoza ndani ya siku mbili |
| Kununua kwa wingi | Nunua Julai hadi Septemba, hifadhi mahindi mzima si mchanganyiko | Mahindi mzima hukaa miezi sita, mchanganyiko hauwezi |
13Gharama na kulinganisha
| Malighafi | Bei kwa kilo (TSh) | Inapatikana wapi |
|---|---|---|
| Mahindi yaliyosagwa | 750 – 900 | Soko la kijiji, mashine ya kusaga |
| Pumba za mahindi | 400 – 600 | Mashine ya kusaga |
| Pumba za mpunga | 300 – 450 | Mashine ya kukoboa mpunga |
| Mihogo mikavu | 450 – 700 | Soko la kijiji |
| Mashudu ya alizeti | 800 – 1,000 | Mashine ya mafuta ya alizeti |
| Mashudu ya soya | 2,000 – 2,400 | Maduka makubwa ya pembejeo mjini |
| Mashudu ya pamba | 700 – 900 | Vinu vya pamba, kanda ya ziwa |
| Machicha ya pombe mabichi | 100 – 200 | Viwanda vidogo vya pombe za kienyeji |
| Dagaa waliosagwa | 4,000 – 5,000 | Soko la samaki, wachuuzi wa ziwa |
| Unga wa samaki | 4,500 – 6,000 | Maduka ya pembejeo |
| Unga wa mifupa | 1,200 – 1,800 | Machinjio, maduka ya pembejeo |
| Chokaa ya kulisha | 500 – 800 | Maduka ya pembejeo na ya ujenzi |
| DCP | 3,000 – 4,000 | Maduka makubwa ya pembejeo |
| Molasi | 600 – 900 | Viwanda vya sukari, maduka ya pembejeo |
| Chumvi ya mezani | 900 – 1,200 | Duka lolote |
| Premix ya nguruwe | 12,000 – 18,000 | Maduka makubwa ya pembejeo |
| Lysine | 20,000 – 25,000 | Maduka makubwa ya pembejeo |
| Maganda ya mayai, majani, mabaki ya hoteli | bure | Nyumbani, shambani, mjini |
Kilo mia moja ya Grower: kulinganisha njia tatu
| Njia | Gharama ya kilo 100 | Gharama kwa kilo | Unaokoa |
|---|---|---|---|
| Kununua gunia la kiwandani | TSh 160,000 | TSh 1,600 | — |
| Toleo la 1, formula kamili | TSh 114,000 | TSh 1,140 | TSh 46,000 |
| Toleo la 2, formula ya kijijini | TSh 99,000 | TSh 990 | TSh 61,000 |
Bei hutofautiana kwa msimu na kwa mkoa. Msimu wa mavuno bei ya mahindi hushuka kwa asilimia thelathini. Kanda ya ziwa dagaa ni nafuu. Mikoa ya kusini mashudu ya alizeti ni nafuu. Fanya hesabu yako mwenyewe kwa bei za sokoni lako.
Hesabu ya kuokoa kwa mwaka
Nguruwe kumi kwa mzunguko, mizunguko miwili kwa mwaka, ni kilo elfu tano na mia nne za chakula. Tofauti ya shilingi mia sita na kumi kwa kilo kati ya kununua gunia la kiwandani na kuchanganya toleo la kijijini ni shilingi milioni tatu na laki tatu kwa mwaka.
14Neno la mwisho
Anza kidogo. Changanya kilo kumi mara ya kwanza, si kilo mia. Mpe nguruwe mmoja kwa siku saba na uangalie. Ukiona anakula vizuri na kinyesi ni kigumu, endelea. Ukiona anaharisha au anakataa chakula, rudi kwenye jedwali na uangalie ulipokosea.
Pima nguruwe wako. Kama huna mizani, pima kifua kwa kamba: pima mzunguko wa kifua nyuma ya miguu ya mbele kwa inchi, uzidishe kwa mzunguko wenyewe mara mbili, kisha zidisha kwa urefu kutoka masikioni hadi mkiani, kisha gawanya kwa mia nne. Utapata pauni, gawanya kwa mbili na robo upate kilo. Andika kila wiki mbili.
Weka daftari. Tarehe ya kuchanganya, kiasi cha kila malighafi, bei uliyolipa, na uzito wa nguruwe. Baada ya mzunguko mmoja utakuwa na taarifa zako mwenyewe zilizo bora kuliko ushauri wowote wa kitabu.
Kwa maswali na ushauri wa ziada, piga simu au tuma ujumbe wa WhatsApp: 0620 339 260.
15Maswali yanayoulizwa sana
Nguruwe anakula chakula kiasi gani kwa siku?
Inategemea uzito. Weaner wa kilo nane hadi ishirini hula kilo 0.6 hadi 1.0. Grower wa kilo ishirini hadi hamsini hula kilo 1.2 hadi 2.0. Finisher wa kilo hamsini hadi tisini hula kilo 2.2 hadi 3.0. Jike anayenyonyesha hula kilo nne hadi sita.
Naweza kumpa nguruwe mabaki ya hotelini?
Ndiyo, lakini lazima uyachemshe kwa dakika thelathini kamili kabla ya kuwapa. Hii huua virusi vya homa ya nguruwe ya Afrika. Usiwape mabaki yenye nyama ya nguruwe hata yakichemshwa.
Protini ngapi kwa nguruwe anayekua?
Asilimia kumi na sita hadi kumi na nane kwa nguruwe wa kilo ishirini hadi hamsini. Baada ya kilo hamsini shuka hadi asilimia kumi na nne.
Naweza kuchanganya chakula cha nguruwe bila premix?
Ndiyo. Tumia toleo la kijijini. Badala ya premix weka kilo mbili za majani ya mlonge, matembele au mihogo yaliyokaushwa kivulini na kusagwa kwa kila kilo mia. Usitumie premix ya kuku.
Nguruwe anachukua muda gani kufikia kilo tisini?
Kwa formula kamili, miezi mitano na nusu hadi sita. Kwa formula ya kijijini, miezi saba. Kwa pumba peke yake, miezi kumi au zaidi.
Kwa nini nguruwe wangu anakula sana lakini hakui?
Mara nyingi ni protini kidogo. Pumba za mahindi zina protini ya asilimia kumi na mbili tu, na lysine kidogo sana. Ongeza mashudu ya alizeti au dagaa. Sababu nyingine ni minyoo, hivyo mpe dawa ya minyoo kila miezi mitatu.
Ni gharama kiasi gani kuchanganya kilo mia mwenyewe?
Kwa bei za wastani, toleo kamili la Grower ni takribani shilingi laki moja na elfu kumi na nne. Toleo la kijijini ni takribani elfu tisini na tisa. Gunia la kiwandani la kiasi hicho ni takribani laki moja na elfu sitini.
Naweza kutumia mihogo badala ya mahindi?
Ndiyo, lakini isizidi robo ya mchanganyiko kwa nguruwe wakubwa, na kilo nane tu kwa vitoto. Loweka mihogo siku tatu ukibadilisha maji, kisha anika juani kuondoa sumu. Ongeza dagaa kilo mbili kwa sababu mihogo haina protini.